RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kukutana
na wabunge wa CCM kwa siku mbili mfululizo kuanzia Mei 18 hadi 19,
mwaka huu, ikiwa ni kikao cha kazi na kushauriana juu ya utekelezaji wa
Ilani ya CCM nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa
ya CCM, Nape Nnauye, alisema katika kikao hicho, Rais Kikwete atafuatana
na wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho.
“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais
kukutana na wabunge wa CCM kwa muda huo wa siku mbili, na hoja
zitakazojadiliwa ni nyingi lakini kubwa ni namna utekelezaji wa Ilani ya
CCM ulipofikia, changamoto zake na namna ya kuzitatua,” alisema Nape.
Alisema katika mkutano huo, wabunge hao
watapata fursa ya kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa Ilani na nini
kifanyike kuitekeleza ipasavyo kwa faida ya Watanzania.
“Naomba niweke wazi kuwa kikao hiki
hakitakuwa na uhusiano wowote wa kudhibitiana, hapa kitakachofanyika ni
kushauriana na wabunge wetu, mwisho wa siku atakayefaidika ni mwananchi
wa kawaida,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Nape alisema baada ya
mkutano huo, Kamati Kuu ya CCM (CC) itakutana katika mkutano wake wa
kawaida, Mei 20 hadi 21.
Akizungumzia yaliyojiri katika mkutano
wa siku moja wa CC uliomalizika juzi, Nape alisema CC, pamoja na mambo
mengine, ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi, kuhusu tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Alisema pamoja na kuridhika na hatua
zilizochukuliwa baada ya tukio hilo, ilililaani kutokana na kurudisha
nyuma maendeleo ya nchi na kuielekeza Serikali, ifanye uchunguzi na
upelelezi wake kwa kasi ili kukamata wahusika wa matukio ya uvunjifu wa
amani nchini.
“Tumeielekeza Serikali iongeze kasi ya
kusaka na kuwakamata wahusika wa tukio hili la Arusha na isishughulikie
matawi pekee, bali itafute mizizi na kuing’oa ili liwe fundisho kwa
wengine wenye nia hiyo,” alisisitiza.
HISANI YA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment