Kocha mpya wa maafande wa jeshi la kujenga taifa wa mkoani Pwani, JKT Ruvu, Keny Mwaisabula “Mzazi” kesho anatarajia kuanza mazoezi na kikosi cha timu hiyo kujiandaa na kipute cha funga pazia la ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya watengeneza sukari wa Mtibwa Sugar wenye makazi yao mashamba ya miwa Turiani Mkoani Morogoro.
Mwaisabula ameipasha FULLSHANGWE kuwa tayari amemwaga wino katika karatasi ya mkataba wa kuwanoamaafande hao wa jeshi na sasa hesabu zake ni msimu ujao wa ligi kuu unaotarajia kuanza mwezi wa nane mwaka huu.
“Kimsingi JKT Ruvu nina mkataba nao, naanza mazoezi mepesi kuwaandaa kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa, vijana kiukweli ni wazuri sana ila kuna mambo madogo wanakosa”. Alisema Mwaisabula maarufu kwa jina la “Mzazi”.
Kocha huyo mwenye historia ya kuzifundisha timu nyingi wakiwemo mabingwa wa sasa wa ligi kuu bara, klabu ya Yanga ya Dar es salaam, aliongeza kuwa kikosi cha maafande hao ni kizuri, wachezaji wanaweza kucheza mpira lakini wamekosa masaada wa kisaikolijia na hilo ndio jukumu mojawapo kwake kwa sasa.
“Timu ni nzuri, natakiwa kuwajenga kisaikolojia ili wajiamini zaidi, walipatwa na mshituko baada ya Kilinda kuwaacha katika kipindi kigumu, lakini naamini nitaweza kuwarudisha katika soka la ushindani kama misimu ya nyuma”. Alisema Mwaisabula.
Mwaisabula alisisitiza kuwa baada ya msimu huu wa ligi kuu kumalizika atakaa chini na kuandaa ripoti yake ambayo itajumuisha mapendekezo ya marekebisho ya kikosi ili aongeze bunduki kali za msimu ujao.
Pia alisema anafurahishwa sana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa timu hiyo ingawa amekaa kwa muda mfupi.
“Viongozi wangu Wanaonesha upendo na mshikamano mkubwa kwangu, nitawalipa fadhila kwa kuunda kikosi kikali cha kushindana msimu ujao”. Alisema Mwaisabula.
hisani ; fullshangwe
No comments:
Post a Comment