Sunday, May 12, 2013
LWAKATARE KUACHIWA LEO !
HATMA ya dhamana ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare itajulikana leo iwapo mawakili wake watakuwa wamekamilisha masharti yanayotakiwa.
Wiki iliyopita Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lawrance Kaduri alimfutia Lwakatare mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili.
Jaji Kaduri alitoa uamuzi huo kutokana na ombi la mawakili wa Lwakatare; Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabere Marando la kutaka mahakama hiyo ipitie mwenendo mzima wa majalada ya kesi Na. 37 na 6 za mwaka huu zilizopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi alitumia madaraka yake kinyume cha sheria kuifuta kesi namba 37 ya mwaka huu.
Makosa yaliyofutwa ni la kula njama lililokuwa likiwakabili washtakiwa wote ambalo ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha sheria ya kuzuia ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002, ambapo walidaiwa kutaka kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Denis Msaki kinyume cha kifungu cha 4(2)(c) (iii) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002.
Shitaka la tatu ni la kupanga kufanya makosa ya ugaidi kinyume cha kifungu cha 59(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msaki kinyume cha kifungu 4(2)(c) (iii) cha sheria ya kuzuia ugaidi.
Shitaka la nne, ambalo linamkabili Lwakatare pekee, ni la kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume cha kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi, kwamba Desemba 28 mwaka jana, akiwa ni mmiliki wa nyumba iliyopo Kimara King’ong’o kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa kikao baina yake na Joseph Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki.
Jaji Kaduri alisema amekubaliana na hoja ya mawakili hao kuwa shitaka la pili, tatu na la nne hayaoneshi kama Lwakatare alikuwa na nia ya kutenda kosa la ugaidi, hivyo atabakia na shtaka la kwanza ambalo ni kula njama kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Msaki.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama inatoa amri ya kumfutia Lwakatare mashitaka matatu, yaani kosa la pili, tatu na la nne kwa sababu Jamhuri imeshindwa kuonesha maelezo yanayotesheleza kumshitaki Lwakatare kwa kesi ya ugaidi.
“Naamuru jalada la kesi ya msingi lilirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya mshtakiwa kuendelea kushtakiwa kwa kosa moja la kula njama ambalo linaangukia katika sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002,” alisema Jaji Kaduri.
Maandalizi ya dhamana
Wakizungumza na Tanzania Daima, mawakili wa Lwakatare, Kibatara na Marando, walisema mwishoni mwa wiki walikuwa wakifanya mchakato wa kupata hukumu ya Mahakama Kuu ili waipeleke Mahakama ya Kisutu.
Walisema mchakato huo ukikamilika watawasilisha hoja ya kutaka mteja wao apewe dhamana kwa hakimu anayeiendesha kesi hiyo ambaye ndiye atakayekuwa na uamuzi.
na Josephat Isango
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment