Kwa siku za karibuni viongozi mbalimbali wa kitaifa na wastaafu wamekuwa wakitoa matamko ya kusisitiza amani nchini.
Dodoma/Pwani.Wakati Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela ameonya Watanzania kuhusu mpasuko wa kidini akibainisha kuwa utaigawa nchi vipande vipande, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ametoa wito maalumu akiwataka waumini wa dini tofauti kuvumiliana.
Malecela na Mwinyi walitoa kauli hizo mjini Dodoma na Kibaha, Pwani jana kwa nyakati tofauti, wote wakiwa na nia ya kusisitiza ulinzi wa amani ya nchi inayoanza kutetereka.
Kauli ya Malecela
Malecela alisema kwa namna ilivyo sasa, Tanzania imekuwa ni tofauti na ile aliyoanza kuiona yeye katika kipindi cha uhuru kwenye miaka ya 1960 wakati huo nchi ikiwa moja na watu wake wakiwa ni wamoja.
“Msipokuwa makini na amani yenu, nchi hii mtaigawa vipande vipande na kamwe amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa mambo ya kusingiziana, badala yake tusaidiane sisi kwa sisi, na sisi na viongozi,” alisema.
Onyo la Malecela limekuja kutokana na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mpasuko wa kidini unaoanza kujitokeza nchini.
Malecela alieleza wasiwasi wake juu ya tofauti za kidini katika ibada maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika Kanisa Anglikana Chiwondo lililoko kijiji cha Hombolo katika Manispaa ya Dodoma.
Anafuata nyayo za viongozi wa kitaifa walioonya masuala ya udini kama Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Marais wastaafu, Mwinyi na Benjamin Mkapa pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Alisema waliovamia na kupiga bomu kanisani Arusha ambapo Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla alinusurika kuuawa, si wajinga na wanaweza kufanya mambo kama hayo eneo lolote nchini.
“Kujenga nchi ni kazi ngumu sana lakini kuibomoa ni kitendo cha muda mfupi ambacho kinaweza kufanyika kwa kutumia sekunde chache ni lazima kuisaidia serikali katika kuitafuta amani,” aliongeza Malecela.
Malecela ameonya baadhi ya watu kutochukua sheria mikononi kuhusu yale yanayowapata na badala yake waiachie Serikali yao kufanya uamuzi wa nini kifanyike ili amani ibaki.
No comments:
Post a Comment