Wednesday, May 15, 2013

Serikali kutoa tamko la viroba



WIZARA ya Viwanda na Biashara itakaa na Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine kuchambua na kujadili athari zinazodaiwa kusababishwa na pombe kali maarufu kama viroba kabla ya kutoa tamko.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema jana bungeni, kwamba wizara yake itakaa kujadiliana na Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufikia uamuzi muafaka. Dk Kigoda alisema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2013/14.
Uamuzi huo wa wizara unatokana na malalamiko yaliyotolewa wiki iliyopita na Mbunge wa Viti Maalumu, Lediana Mng’ong’o (CCM) akishutumu pombe hiyo inayowekwa kwenye mifuko, kwamba imechangia kuharibu watoto, vijana na pia kusababisha ajali kutokana na kununuliwa na kunywewa kiholela. Mbunge huyo alisema baadhi ya madereva wamekuwa wakiendesha magari huku wakinywa pombe hiyo.
“Tunaomba mpige marufuku viroba. Pombe hii imeharibu watoto na vijana katika shule; madereva wanaendesha magari wanakunywa viroba,” alisema Mng’ong’o na kuhoji kama Kenya na Uganda wamemudu kuipiga marufuku, iweje nchini ishindikane.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, wakati akijumuisha michango ya wabunge, alisema wizara yake haiwezi kutamka kama pombe hiyo ipigwe marufuku kwa kuwa suala hilo liko mikononi mwa Wizara ya Viwanda.
Wakati huo huo, Sheria ya Biashara ya Chuma Chakavu iko mbioni kutungwa kutokana na muswada husika kufanyiwa maboresho kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema jana bungeni kwamba wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha uandaaji wa rasimu ya sheria ya biashara hiyo baada ya kujadiliwa katika ngazi ya makatibu wakuu.
“Muswada wa kutunga sheria hiyo unafanyiwa maboresho ili kuwasilishwa Baraza la Mawaziri kwa uamuzi na hatimaye Kamati ya Sheria na Katiba kuwasilishwa rasmi bungeni,” alisema Dk Kigoda.
Dk Kigoda alisema katika bajeti ya mwaka 2013/14 wizara yake inaendelea kukamilisha sheria na kuandaa kanuni za biashara ya chuma chakavu.
Katika mwaka ujao wa fedha, wizara na taasisi zilizo chini yake, imeomba kutengewa Sh 108,502,631,820 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kuendeleza sekta ya viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo na biashara ndogo. Kati ya fedha hizo, Sh 29,665,989,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 78,836,642,820 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment