Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amelazimika kukatiza vikao vya Bunge kwa muda mkoani Dodoma, na kurejea Dar es Salaam kupanga mikakati ya timu yake kuikabili Yanga keshokutwa.
Yanga na Simba zitacheza Jumamosi katika mechi ya marudiano na ya kufunga dimba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo la watani wa jadi litakuwa la kulinda heshima kwani tayari Yanga imetawazwa mabingwa wapya wakiipoka kombe Simba, na pia mshindi wa pili amejulikana kuwa ni Azam FC kwa mara ya pili mfululizo.
Hata hivyo, kutokana na utani wa jadi kati ya miamba hiyo na ukweli kuwa vikosi viwili hivyo vina sura tofauti, pambano hilo linasubiriwa kwa hamu.
Wakati Yanga ikijivunia wachezaji wazoefu na chipukizi kadhaa, Simba imeamua kutumia wachezaji chipukizi mwishoni mwa msimu baada ya kuwatema wachezaji wake wengi wazoefu.
Aidha, Yanga inalichukulia kwa uzito mkubwa pambano hilo ikipania kurejesha kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata kwa Simba katika mechi ya mwisho mwaka jana.
Kutokana na uzito huo, Rage jana aliondoka hapa kurejea Dar es Salaam ambako inaelezwa kuwa alitarajiwa kuongoza kikao kizito jana jioni kabla ya baadhi ya vigogo wa timu hiyo kwenda kambini Unguja.
Wakati hayo yakiendelea kwa upande wa Simba, tayari baadhi ya vigogo wa Yanga, Seif Magari na Abdallah Bin Kleb waliondoka jana kwenda Pemba ilipoweka kambi timu yao.
Rage, ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alithibitisha jana kurejea Dar es Salaam, lakini akasema atakuwapo Dodoma leo.
“Ni kweli hivi sasa naelekea Dar, lakini nitarudi kesho, nina kikao muhimu leo jioni (jana),” alisema Rage na alipoulizwa kama ni kuhusu pambano la Simba na Yanga, alicheka na kueleza “ni kikao muhimu cha kazi.”
Inaaminika kuwa Rage alikwenda kuonana na Kundi la Marafiki wa Simba ‘Friends of Simba’ kupanga mkakati wa kuibuka na ushindi keshokutwa.
Wakati Rage akirejea Dar es Salaam kwa muda, wabunge wa Yanga jana walijitokeza kujibu mapigo ya wenzao wa Simba yaliyotolewa juzi na Profesa Juma Kapuya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa, alitangaza jana bungeni kuwa ubingwa wa Yanga utanoga kwa kuifunga Simba.
“Nampongeza Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji kwa Yanga kutwaa ubingwa, lakini ubingwa utanoga kama tutaifunga Simba na hivyo itafanya wamfukuze vizuri Mwenyekiti wao Rage ambaye yupo hapa,” alisema Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini.
Awali, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akiongoza kikao cha asubuhi, alimpongeza Manji kwa Yanga kutwaa ubingwa, akisema amefanya hivyo kwa kuwa mabingwa hao wako jimboni mwake.
Yanga na Simba zote ziko visiwani Zanzibar, kwa vijana wa Jangwani kujifua Pemba na vijana wa Msimbazi, kujifua Unguja, tayari kwa pambano ambalo mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro atapuliza filimbi.