Wednesday, May 15, 2013

Yanga, Simba presha tup



HOMA ya pambano la watani wa jadi, Yanga na Simba imezidi kupanda baada ya vigogo wa timu hizo kufunga safari katika kambi zao zilizopigwa Pemba na Uguja, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amelazimika kukatiza vikao vya Bunge kwa muda mkoani Dodoma, na kurejea Dar es Salaam kupanga mikakati ya timu yake kuikabili Yanga keshokutwa.
Yanga na Simba zitacheza Jumamosi katika mechi ya marudiano na ya kufunga dimba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo la watani wa jadi litakuwa la kulinda heshima kwani tayari Yanga imetawazwa mabingwa wapya wakiipoka kombe Simba, na pia mshindi wa pili amejulikana kuwa ni Azam FC kwa mara ya pili mfululizo.
Hata hivyo, kutokana na utani wa jadi kati ya miamba hiyo na ukweli kuwa vikosi viwili hivyo vina sura tofauti, pambano hilo linasubiriwa kwa hamu.
Wakati Yanga ikijivunia wachezaji wazoefu na chipukizi kadhaa, Simba imeamua kutumia wachezaji chipukizi mwishoni mwa msimu baada ya kuwatema wachezaji wake wengi wazoefu.
Aidha, Yanga inalichukulia kwa uzito mkubwa pambano hilo ikipania kurejesha kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata kwa Simba katika mechi ya mwisho mwaka jana.
Kutokana na uzito huo, Rage jana aliondoka hapa kurejea Dar es Salaam ambako inaelezwa kuwa alitarajiwa kuongoza kikao kizito jana jioni kabla ya baadhi ya vigogo wa timu hiyo kwenda kambini Unguja.
Wakati hayo yakiendelea kwa upande wa Simba, tayari baadhi ya vigogo wa Yanga, Seif Magari na Abdallah Bin Kleb waliondoka jana kwenda Pemba ilipoweka kambi timu yao.
Rage, ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alithibitisha jana kurejea Dar es Salaam, lakini akasema atakuwapo Dodoma leo.
“Ni kweli hivi sasa naelekea Dar, lakini nitarudi kesho, nina kikao muhimu leo jioni (jana),” alisema Rage na alipoulizwa kama ni kuhusu pambano la Simba na Yanga, alicheka na kueleza “ni kikao muhimu cha kazi.”
Inaaminika kuwa Rage alikwenda kuonana na Kundi la Marafiki wa Simba ‘Friends of Simba’ kupanga mkakati wa kuibuka na ushindi keshokutwa.
Wakati Rage akirejea Dar es Salaam kwa muda, wabunge wa Yanga jana walijitokeza kujibu mapigo ya wenzao wa Simba yaliyotolewa juzi na Profesa Juma Kapuya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa, alitangaza jana bungeni kuwa ubingwa wa Yanga utanoga kwa kuifunga Simba.
“Nampongeza Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji kwa Yanga kutwaa ubingwa, lakini ubingwa utanoga kama tutaifunga Simba na hivyo itafanya wamfukuze vizuri Mwenyekiti wao Rage ambaye yupo hapa,” alisema Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini.
Awali, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akiongoza kikao cha asubuhi, alimpongeza Manji kwa Yanga kutwaa ubingwa, akisema amefanya hivyo kwa kuwa mabingwa hao wako jimboni mwake.
Yanga na Simba zote ziko visiwani Zanzibar, kwa vijana wa Jangwani kujifua Pemba na vijana wa Msimbazi, kujifua Unguja, tayari kwa pambano ambalo mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro atapuliza filimbi.

BABA JONII KUTAMBULISHA SINGLES

Adam Mchomvu a.k.a baba jonii Radio presenter clouds fm mwenye crown ya best presenter, anatarajia kutoa mixtape yenye  ngoma kumi na nane LEO  alioshirikiana na wasanii mbali mbali kama Jose Mtambo, Banana Zorro, Illimatix, Cliff mitindo, G.nako, Nikk war 2, Babuu war kitaa, TID, na wasanii wengine wengi kama zawadi kwa mashabiki wake ibaki kama kumbukumbu kwa kile anachokifanya hewani (on air) ... mixtape itaingia kitaani soon baada kupreview ngoma hizo ndani ya double XL (XXL) kuanzia saa tisa alasiri kwa hot 3 @ 3 ..... big up baba la baba!

Wabunge CCM kuteta na Kikwete



RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kukutana na wabunge wa CCM kwa siku mbili mfululizo kuanzia Mei 18 hadi 19, mwaka huu, ikiwa ni kikao cha kazi na kushauriana juu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, alisema katika kikao hicho, Rais Kikwete atafuatana na wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho.
“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais kukutana na wabunge wa CCM kwa muda huo wa siku mbili, na hoja zitakazojadiliwa ni nyingi lakini kubwa ni namna utekelezaji wa Ilani ya CCM ulipofikia, changamoto zake na namna ya kuzitatua,” alisema Nape.
Alisema katika mkutano huo, wabunge hao watapata fursa ya kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa Ilani na nini kifanyike kuitekeleza ipasavyo kwa faida ya Watanzania.
“Naomba niweke wazi kuwa kikao hiki hakitakuwa na uhusiano wowote wa kudhibitiana, hapa kitakachofanyika ni kushauriana na wabunge wetu, mwisho wa siku atakayefaidika ni mwananchi wa kawaida,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Nape alisema baada ya mkutano huo, Kamati Kuu ya CCM (CC) itakutana katika mkutano wake wa kawaida, Mei 20 hadi 21.
Akizungumzia yaliyojiri katika mkutano wa siku moja wa CC uliomalizika juzi, Nape alisema CC, pamoja na mambo mengine, ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, kuhusu tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Alisema pamoja na kuridhika na hatua zilizochukuliwa baada ya tukio hilo, ilililaani kutokana na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi na kuielekeza Serikali, ifanye uchunguzi na upelelezi wake kwa kasi ili kukamata wahusika wa matukio ya uvunjifu wa amani nchini.
“Tumeielekeza Serikali iongeze kasi ya kusaka na kuwakamata wahusika wa tukio hili la Arusha na isishughulikie matawi pekee, bali itafute mizizi na kuing’oa ili liwe fundisho kwa wengine wenye nia hiyo,” alisisitiza.

HISANI YA HABARI LEO

Serikali kutoa tamko la viroba



WIZARA ya Viwanda na Biashara itakaa na Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine kuchambua na kujadili athari zinazodaiwa kusababishwa na pombe kali maarufu kama viroba kabla ya kutoa tamko.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema jana bungeni, kwamba wizara yake itakaa kujadiliana na Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufikia uamuzi muafaka. Dk Kigoda alisema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2013/14.
Uamuzi huo wa wizara unatokana na malalamiko yaliyotolewa wiki iliyopita na Mbunge wa Viti Maalumu, Lediana Mng’ong’o (CCM) akishutumu pombe hiyo inayowekwa kwenye mifuko, kwamba imechangia kuharibu watoto, vijana na pia kusababisha ajali kutokana na kununuliwa na kunywewa kiholela. Mbunge huyo alisema baadhi ya madereva wamekuwa wakiendesha magari huku wakinywa pombe hiyo.
“Tunaomba mpige marufuku viroba. Pombe hii imeharibu watoto na vijana katika shule; madereva wanaendesha magari wanakunywa viroba,” alisema Mng’ong’o na kuhoji kama Kenya na Uganda wamemudu kuipiga marufuku, iweje nchini ishindikane.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, wakati akijumuisha michango ya wabunge, alisema wizara yake haiwezi kutamka kama pombe hiyo ipigwe marufuku kwa kuwa suala hilo liko mikononi mwa Wizara ya Viwanda.
Wakati huo huo, Sheria ya Biashara ya Chuma Chakavu iko mbioni kutungwa kutokana na muswada husika kufanyiwa maboresho kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema jana bungeni kwamba wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha uandaaji wa rasimu ya sheria ya biashara hiyo baada ya kujadiliwa katika ngazi ya makatibu wakuu.
“Muswada wa kutunga sheria hiyo unafanyiwa maboresho ili kuwasilishwa Baraza la Mawaziri kwa uamuzi na hatimaye Kamati ya Sheria na Katiba kuwasilishwa rasmi bungeni,” alisema Dk Kigoda.
Dk Kigoda alisema katika bajeti ya mwaka 2013/14 wizara yake inaendelea kukamilisha sheria na kuandaa kanuni za biashara ya chuma chakavu.
Katika mwaka ujao wa fedha, wizara na taasisi zilizo chini yake, imeomba kutengewa Sh 108,502,631,820 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kuendeleza sekta ya viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo na biashara ndogo. Kati ya fedha hizo, Sh 29,665,989,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 78,836,642,820 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.

Monday, May 13, 2013

Pochi ya Mwanamke

image
Pochi ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanamke. Pochi zipo za aina, rangi, ukubwa na matumizi mbali mbali. Ni nadra sana kukutana na binti au mama anayetembea bila pochi, na kwa wengine maisha yao yote wanatembea nayo kwenye pochi.
Kuna vitu muhimu ambavyo ni lazima kila mwanamke akumbuke kutembea navyo kwenye pochi, na kuna vingine ni vyema kuwa navyo lakini sio lazima.

Muhimu
1. Pini
2. Sindano na uzi
3. Vifungo
4. Dawa yoyote ambayo unaitumia na kuihitaji
5. Kitambulisho
6. Pedi
7. Kalamu na notebook

Ukipenda
1. Perfume
2. Lip shiner / lip stick
3. Poda
4. Kitana
5. Khanga / mtandio
6. Kadi ya benki
7. Sandals kama unavaa viatu virefu

Tibu chunusi kwa kutumia limau!



Limau kulina tindikali aina ya citric ambayo inasaidia kuponya chunusi. Vilevile tunda hilo lina Vitamin C ambayo ni muhimu katika kuifanya ngozi iwe na afya wakati alkali inayopatikana katika limau nayo husaidia kuua vijidudu vinavyosababisha chunusi.
Kunywa juisi ya limau kama chakula cha kwanza asubuhi kunaaminika kusadia kuboresha ngozi.
Jinsi ya kutengeneza nyumbani mchanganyiko wa limau kwa ajili ya kutibu chunusi:
• Kwa kutumia pamba paka maji ya limau katika sehemu yenye chunusi na wacha kwa usiku kucha.
• Safisha kwa maji safi asubuhi inayofuata.
• Ingawa unaweza ukahisi kuwashwa wakati unapopatumia mchanganyiko huo juu ya ngozi mara ya kwanza, lakini baadaye hali hiyo huzoeleka.
Au

1. Changanya maji ya limau ulioyakamu kutoka katika kipnde kimoja cha limao na changanya na maji ya waridi (rose water) au asali nyepesi kwa kiwango hicho hicho.
2. Paka mchanganyiko huo katika sehemu za ngozi zenye chunusi na subiri kwa muda usiopungua nusu saa mpaka saa lizima.
3. Baadye osha kwa maji.
Mchanganyiko huu unapaswa kupakwa mara mbili kwa siku, bora utumiea asubuhi na jioni.
Muhimu: kutumia mchanganyiko huu hakuna madhara na ni wa asilia, lakini iwapo chunusi zinazidi au kuna vidonda vinavyoambatana na chunusi ni bora upate uchauri wa daktari kwanza.

Ngozi zenye mafuta na jinsi ya kuzitunza



Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang'ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.
Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:
• Kuridhi.
• Lishe.
• Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
• Ujauzito.
• Vidonge vya kuzuia mimba.
• Baadhi ya vipodozi .
• Hali ya unyevu (humidity) na hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta
Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-
1. Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.
2. Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.
3. Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipotze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.
4. Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.
5. Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.
6. Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.
7. Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.
8. Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.
9. Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.